SIMBA – TUZO ya Mshambuliaji Bora wa mwaka – MO SIMBA AWARDS

John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wameteuliwa kuwania tuzo ya mshambuliaji bora wa mwaka

Bocco, Kagere na Okwi wameongoza vyema safu ya ushambuliaji ya Simba wakifunga mabao 50 kati ya 72 yaliyofungwa kwenye ligi

Kagere anaongoza mbio za kuwania kiatu cha dhahabu ligi kuu ya Tanzania Bara akiwa amefunga mabao 20

Mshambuliaji huyo pia ndiye kinara wa mabao wa kikosi cha Simba katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika ambayo Simba imetolewa hatua ya robo fainali amefunga mabao sita

Bocco na Okwi wamefunga mabao 15 kila mmoja kwenye ligi kuu ya Tanzania Bara

Kupiga kura tembelea tovuti rasmi ya MO SIMBA AWARDS kwa kubonyeza HAPA

SIMBA Yamalizana na Bocco

Klabu ya Simba inaendelea na mchakato wa kuhuisha mikataba ya wachezaji wake ambayo inamlizika na tayari imemalizana na nahodha wake John Bocco

Taarifa za uhakika ni kwamba Bocco amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kukipiga Msimbazi hadi mwaka 2021

Bocco aliyeifungia Simba mabao 15 kwenye ligi ya Tanzania Bara msimu huu, alikuwa akiwaniwa na timu yake ya zamani Azam FC

Azam Fc inadaiwa kuwashawishi Aishi Manula, Erasto Nyoni, John Bocco na Shomaria Kapombe wasaini kunako klabu hiyo waliyokuwa wakicheza kabla ya kusajiliwa na Simba mwaka juzi

Msimu uliopita Bocco aliibuka kuwa mchezaji bora wa Simba na msimu huu ameteuliwa kuwania tuzo hiyo sambamba na Meddie Kagere na Clatous Chama

Zoezi la kuchagua mchezaji bora wa msimu huu tayari limeanza, kura zinapigwa kupitia tovuti rasmi ya Mo Simba Awards

Bonyeza HAPA kumpigia kura Bocco kama unadhani anastahili kuwa mchezaji bora wa Simba msimu huu

CAF Yatangaza Gharama za Tiketi Nchini Misri

Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) limetangaza gharama za tiketi za kutazama mechi za Fainali za Africa (AFCON) zinazotarajia kuanza mwezi ujao nchini Misri.

Kwa upande wa Shrikisho la soka nchini TFF limethibitisha taarifa hiyo, ikisema kuwa CAF imetangaza gharama hizo kwa madaraja mbalimbali, kwenye michezo ya hatua ya makundi ambayo itahusisha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) tiketi za daraja la kwanza ni USD 29 ambayo ni sawa na takribani sh 66,700 za Kitanzania, tiketi za daraja la pili ni USD 18 ambazo ni sawa na sh 41,403 tiketi za daraja la tatu ni USD 6.

Katika hatua ya makundi, Taifa Stars itacheza michezo mitatu ambapo itaanza dhidi ya Senegal ikifuatiwa na mchezo dhidi ya Kenya na kumalizia hatua hiyo kwa kucheza na Algeria

Aidha, Kwenye hatua ya robo fainali gharama ya tiketi daraja la kwanza ni USD 35 ambayo ni takribani sh 80,521 kwa daraja la pili ni USD 24 na daraja la tatu ni USD 12.

Hatua ya nusu fainali, tiketi daraja la kwanza ni USD 59 ambazo ni sawa na sh 135,700, daraja la pili ikiwa ni USD 29 na daraja la 3 USD 18. Mchezo wa mshindi wa 3 utakua na gharama ya USD 35 kwa daraja la kwanza, USD 24 kwa daraja la 2 na USD 12 daraja la 3.

Mchezo wa fainali, daraja la kwanza ni USD 106 ambazo ni takribani sh 243,800, daraja la 2 ni USD 44 ambazo ni takribani sh 101,200 na daraja la tatu ni USD 24.

Pia TFF imesema kwa yoyote mwenye nia ya kununua tiketi hizo za AFCON awasiliane na shirikisho hilo mapema kabla ya kufungwa kwa muda wa maombi.

MAKAMBO Ajaza Pesa JANGWANI

Yanga imefikia makubaliano na klabu ya Horoya Fc kumuuza mshambuliaji wake Heritier Makambo aliyesaini kunako klabu hiyo mkataba wa miaka mitatu

Habari njema ni kuwa Yanga itafanya biashara ya faida kwani itaingiza zaidi ya Mil 230, ikipata faida ya zaidi ya Mil 170

Makambo alitua Yanga akitokea klabu ya FC Lupopo ya DR Congo kwa dau la takribani Milioni 60

Yanga inaendelea na mchakato wa kukiboresha kikosi chake na bila shaka fedha hizo zitatumia katika usajili unaoendelea

Makambo tayari ametambulishwa kunako klabu ya Horoya Fc, mabingwa wa Guinea

Mkurugenzi wa Ufundi wa Horoya Jaid Martin wiki ijayo atakuwa jijini Dar es Salaam kumalizana na Yanga ili kukamilisha taratibu za mwisho za usajili wa Makambo

Uongozi wa Yanga kupitia Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla amethibitisha kuwa na taarifa ya Makambo kwenda kufanyiwa vipimo vya afya

“Ni kweli Makambo aliondoka juzi na mwalimu Zahera kuelekea Guinea kwa ajili ya vipimo kwa klabu ya Horoya huko Guinea,” amesema Dk Msolla

“Tunasubiri warudi tuitazame ofa yao kisha tufanye biashara. Taarifa za kutambulishwa rasmi sizielewi ila mwalimu akirudi tutaitazama ofa yao kulinganisha na klabu zingine nyingi zinazomtaka kisha tutafanya maamuzi”

ZAHERA : Asaka Mrithi wa MAKAMBO

Baada ya kusambaa kwa taarifa za mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo kusajiliwa na Horoya AC ya Guinea kwa mkataba wa miaka mitatu, Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla alifafanua kuwa dili hilo limeihusisha klabu yake na Makambo aliondoka nchini na Kocha Mwinyi Zahera

Hata hivyo imefahamika Zahera alilekea nchini Bennin ambako amekwenda kufanya mazungumzo na mshambuliaji mwingine

Halitakuwa jambo la kushangaza kama mshambuliaji huyo atakuwa Marcellin Koukpo ambaye alikuja msimu uliopita lakini usajili wake kukwamishwa na wajanja wachache waliokuwa wakitaka ‘ten percent’

Koukpo mshambuliaji wa Kimataifa wa Benin, alikaa nchini kwa zaidi ya wiki mbili kabla ya kuamua kuondoka baada ya kupishana na viongozi wa Yanga

Mshambuliaji huyo alipendekezwa na aliyekuwa kocha wa Yanga msimu uliopita, George Lwandamina na alifanyiwa majaribio na kocha Mwinyi Zahera kabla ya kuibuliwa taarifa za ‘uzushi’ kuwa ameshindwa majaribio

Baada ya kumuuza Makambo, Yanga inaweza kusajili washambuliaji wawili ambapo mmoja anaweza kuwa huyo Mbenin huku timu hiyo ikihusishwa na mshambuliaji wa Gor Mahia Jacques Tuyisenge na Roderick Matuma raia wa Zimbabwe anayekipiga kunako klabu ya Fc Lupopo

Dirisha la usajili litafunguliwa mwezi ujao ambapo uongozi wa Yanga umepania kukiimarisha kikosi chake wakijipanga kutumia kati ya Bil 1.5 hadi Bil 2

Hata hivyo Yanga imedhamiria kukamilisha masuala ya usajili mapema hasa ikizingatiwa Zahera ndiye msimamizi Mkuu wa mchakato huo

Mwanzoni mwa mwezi wa sita Zahera atarejea kwao Congo kwa ajili ya majukumu ya timu ya Taifa kuelekea fainali za AFCON zitakazofanyika Misri kuanzia Juni 21 2019

SIMBA inamkumbuka Patrick Mafisango

Tarehe kama ya leo miaka saba iliyopita, May 17 2012 klabu ya Simba ilipatwa na majonzi makubwa baada ya kumpoteza kiungo wake Patrick Mafisango aliyefariki kwa ajali ya gari

Umauti ulimfika Mafisango kupitia ajali ambayo katika jitihada za kunusuru maisha ya mwendesha pikipiki, gari yake iliingia mtaroni na kusababisha apoteze maisha kutokana na majeraha aliyopata

Kabla ya kuja Tanzania Mafisango alichezea APR ya Rwanda na alipofika nchini alijiunga na Azam Fc kabla ya kusajiliwa na Simba

Mechi ya mwisho Mafisango kuichezea Simba ilikuwa dhidi ya Al Ahly Shandy nchini Sudan katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penalti 9-8, kufuatia sare ya jumla ya 3-3.

Hadi anafariki dunia, Mafisango alikuwa ni tegemeo Simba katika safu ya kiungo

Pamoja na kucheza kama kiungo, Mafisango pia anamudu kucheza nafasi ya beki wa kushoto na beki wa kati

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems ameeleza furaha yake baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems ameeleza furaha yake baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Uhuru

Akizungumza na Wanahabari baada ya mchezo huo, Aussems amesema Simba ilitawala mchezo na ilistahili kuondoka na ushindi mnono

Aidha Aussems amesema ushindi umezidi kuisogeza Simba karibu na ubingwa wa pili mfululizo

“Tulitawala mchezo, tulitengeneza nafasi na tulifanikiwa kufunga. Jambo muhimu tumekaribia lengo letu,” amesema Aussems

KRC GENK anayochezea mtanzania Mbwana Samatta imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi kuu nchini Ubelgiji

Klabu ya KRC GENK anayochezea mtanzania Mbwana Samatta imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi kuu nchini Ubelgiji maarufu kama Belgium Pro League mara baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Anderlecht huku ikisaliwa na mchezo mmoja mkononi.
.
Genk itamaliza mchezo wake wa mwisho ikiwa nyumbani dhidi ya St.Liege.
.
.
Hongera @samagoal77