Simba dimbani leo kuikabili KMC

Kikosi cha Simba leo tena kinashuka katika uwanja wa CCM Kirumba kuikabili KMC kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Baada ya juzi kuichapa Alliance Fc mabao 2-0 kwenye uwanja huo, leo Simba inarejea tena ikiwa na shauku ya kuondoka na alama zote tatu

Kocha Mkuu wa mabingwa hao watetezi Patrick Aussems amesema wanatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa KMC lakini wamejipanga kupata matokeo yatakayowapandisha hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi

Ushindi utaiwezesha Simba kufikisha alama 66 na kuiondoa Azam Fc katika nafasi ya pili kutokana na wingi wa mabao ya kufunga

Katika mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa, Simba ilifanikiwa kuondoka na alama zote tatu kwa ushindi wa mabao 2-1 huku ikifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake

Leo pia Aussems amesema atafanya mabadiliko ya kikosi kwani mchezo wa leo unahitaji uzoefu na ufundi

TMA yatoa tahadhari ujio wa kimbunga Keneth

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetangaza kuwa Kimbunga Kenneth kimeongezeka kasi na kinatarajiwa kufika pwani ya kusini ya Tanzania na kaskazini mwa Msumbiji kuanzia usiku wa leo Alhamisi

Kwa mujibu wa TMA, jana kimbunga hicho kilikuwa kilomita 450 kutoka pwani ya Mtwara na kina kasi ya kilomita 130 kwa saa.

Kimbunga hicho kinatarajiwa kuongeza nguvu zaidi leo Alhamisi mchana ambapo kitakuwa kinasafiri kwa kilomita 170 kwa saa na kitakuwa kilomita 150 kutoka pwani ya Mtwara.

Kwa mujibu wa TMA, eneo husika ambalo kimbunga hicho kitatua litakuwa nchini Msumbiji, kikiwa na kasi ya kilomita 100 kwa saa. Eneo hilo litakuwa kilomita 200 kutoka pwani ya Mtwara.

Hata hivyo, mkoa wa Mtwara na maeneo jirani hususani mikoa ya Lindi na Ruvuma yataathirika pakubwa (athari zinategemewa kufikia umbali mpaka wa kilomita 500 kutoka Mtwara).

TMA imetahadharisha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu na nguvu kubwa (ya upepo na mvua) itakayopelekea madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.

“Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibufu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali. Uharibifu wa mazao mashambani na miundombinu kutokana na mafuriko”

Azam Fc vs Yanga mchezo usiotabirika

Jumatatu ya April 29 Azam Fc na Yanga zitachuana katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Huo utakuwa mchezo wa 19 kwa timu hizo kukutana kwenye ligi katika kipindi cha miaka 10

Katika michezo 18 iliyopita, Yanga na Azam Fc zimekuwa na matokeo sawa ambapo Yanga imeshinda michezo sita, Azam Fc ikishinda sita pia huku zikitoka sare mara sita

Hizi hapa takwimu za matokeo ya michezo iliyopita;

2008/09
Azam 1-3 Yanga (Oktoba 15, 2008)
Yanga 2-3 Azam (Aprili 8, 2009)

2009/10
Azam 1-1 Yanga (Oktoba 17, 2009)
Yanga 2-1 Azam (Machi 7,2010)

2010/11
Azam 0-0 (Okt 24, 2010)
Yanga 2-1 Azam (Machi 30, 2011)

2011/12
Azam 1-0 Yanga (Sept 18, 2011)
Yanga 1-3 Azam (Machi 10, 2012)

2012/13
Azam 0-2 Yanga (Nov 4, 2012)
Yanga 1-0 Azam (Feb 23, 2013)

2013/14
Azam 3-2 Yanga (Sept 22, 2013)
Yanga 1-1 Azam (Machi 19, 2014)

2014/15
Yanga 2-2 Azam (Des 28, 2014)
Azam 2-1 Yanga (Mei 5, 2015)

2015/16
Yanga 1-1 Azam (Okt 17,2015)
Azam 2-2 Yanga (Machi 5, 2016)

2017/2018
Azam fc 1-2 Yanga sc (Junuari 27/1/2017
Yanga 1-3 Azam Fc (May 28/5/2018

Katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita, upinzani wa Yanga na Azam Fc umekuwa ukiongezeka hasa baada ya Azam Fc kuanza utamaduni wa kusajili wachezaji kutoka Yanga

Baada ya Azam Fc kuwasajili Didier Kavumbagu na Frank Domayo, mwaka juzi Yanga ilimnyakua Gadiel Michael

Mwaka jana Azam Fc iliwasajili Donald Ngoma aliyeachwa na Yanga na baadae Obrey Chirwa

Ngoma na Chirwa wanatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya Azam Fc kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Yanga

Chirwa aliifunga Yanga mapema mwaka huu kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi katika mchezo ambao Azam Fc ilishinda mabao 3-0

Hata hivyo Yanga haikupeleka kikosi chake cha kwanza katika michuano hiyo ambayo Azam Fc iliibuka mabingwa

Ni mchezo ambao Yanga inahitaji kupata ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa huku pia ikiiombea Simba iendelee kupunguzwa kasi katika michezo yake ya viporo

Matokeo tofauti na ushindi kwa Yanga huenda yakafifisha nafasi ya kutwaa ubingwa kwa vinara hao wa ligi kuu msimu huu

Azam Fc haina cha kupoteza kwani tayari imeshajiondoa katika kinyan’ganyiro cha kuwania ubingwa ikiweka mkazo zaidi kwenye michuano ya kombe la FA (ASFC)

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema mchezo huo hautakuwa mwepesi kutokana na ubora wa kikosi cha Azam Fc hata hivyo ni matokeo ya ushindi pekee ambayo yanaweza kuwapa nafasi ya kuwa mabingwa

“Hii ni mechi ngumu kwetu, Azam Fc ni timu nzuri ambayo ina ushindani wa hali ya juu. Tunafanya maandalizi maalum ili tuweze kuwafunga,naamini tukishinda tutajiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kuchukua ubingwa,” amesema

Yanga inaongoza ligi ikiwa na alama 74, ikiwa mbele ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama nane

Simba yakamilisha maandalizi ya kuikabili KMC

Kikosi cha Simba leo asubuhi kimefanya mazoezi ya mwisho kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya KMC

Mchezo huo utapigwa kesho Alhamisi kwenye uwanja wa CCM Kirumba

Simba ilishuka katika uwanja huo huo jana kuikabili Alliance Fc katika mchezo ambao Simba ilishinda kwa mabao 2-0

Baada ya mazoezi hayo yaliyosimamiwa na kocha Patrick Aussems, wachezaji walipewa mapumziko kusubiri mchezo huo wa kesho

Ratiba ya mabingwa hao watetezi haitoi nafasi kwa wachezaji kupata mapumziko ya kutosha hivyo benchi la ufundi kulazimika kupunguza muda wa mazoezi ili kuwapumzisha wachezaji

Hii hapa ‘bandika-bandua’ ya michezo ya Simba

Ratiba imebana kwelikweli! Ndio kauli unayoweza kuitumia kwa Simba ambayo imekuwa ikishuka dimbani kila baada ya siku mbili au siku tatu

Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Alliance Fc jana, kesho Simba itashuka tena uwanja wa CCM Kirumba kuikabili KMC katika mchezo mwingine wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Kocha Mkuu wa mabingwa hao watetezi Patrick Aussems amesema ataendelea kufanya ‘rotation’ ya kikosi chake ili kuhakikisha wanafikia malengo ya kutetea ubingwa

Hii hapa ratiba ya Simba kwa michezo iliyobaki mpaka mwishoni mwa msimu;
25/04/19 KMC Vs Simba SC .
27/04/19 Biashara Utd FC Vs Simba Sc.

30/04/19 Simba Sc Vs JKT Tanzania .
03/05/19 Mbeya City FC Vs Simba Sc.
06/05/19 Tanzania Prisons FC Vs Simba SC.

08/05/19 Simba SC Vs Coastal Union.
10/05/19 Simba SC Vs Kagera sugar FC.

13/05/19 Simba SC Vs Azam FC.
16/05/19 Simba SC Vs Mtibwa Sugar FC.

19/05/19 Simba SC Vs Ndanda FC.
22/05/19 Singida United vs Simba Sc.

25/05/19 Simba SC Vs Biashara United.

28/05/19 Mtibwa Sugar FC Vs Simba SC.

Ushindi dhidi ya Alliance umetuongezea morali – Niyonzima

Kiungo Haruna Niyinzima amesema ushindi wa mabao 2-0 waliopata jana dhidi ya Alliance Fc umewaongezea morali wachezaji na wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanatetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Niyonzima aliye katika kiwango bora, aliifungia Simba bao la kwanza na baadae Okwi kuongeza la pili katika kipindi cha pili

“Mchezo haukuwa rahisi hasa kutokana na matokeo tuliyopata kwenye mchezo uliopita, tulikuwa na presha ya kupata ushindi,” amesema Niyonzima

“Tunashukuru tumefanikiwa kuondoka na alama zote tatu, matokeo haya yametuongezea morali ya kufanya vizuri kwenye michezo ijayo”

Akizungumzia ugumu wa ratiba, Niyonzima amesema Simba ilisajili wachezaji 30 hivyo anaamini wataweza kukabiliana na changamoto ya kucheza kila baada ya siku mbili au tatu

“Kocha alituambia atakuwa akifanya mabadiliko ya kikosi ili kuhakikisha kila mchezaji anahusika. Hii ndio faida ya kusajili wachezaji wengi”

“Najua haitakuwa kazi rahisi lakini naamini tutafanikiwa kutetea ubingwa”

Simba imebaki jijini Mwanza ambapo kesho itashuka tena kwenye uwanja wa CCM Kirumba kuikabili KMC

Djuma yamkuta Rwanda, atimuliwa As Kigali

Aliyewahi kuwa kocha Msaidizi wa Simba Masudi Djuma ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo, ametimuliwa klabu ya AS Kigali aliyokuwa akiifundisha

Djuma alijiunga na AS Kigali mwezi Oktoba mwaka jana baada ya uongozi wa Simba kuvunja mkataba wake akituhumiwa kumfanyia hujuma kocha Patrick Aussems

Djuma ameinoa AS KIgali kwa muda wa miezi saba tu akitimuliwa baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo mitano iliyopita bila ya kupata ushindi

Faini zaiandama Yanga

Klabu ya Yanga imetozwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi dhidi ya Ndanda Fc iliyofanyika Aprili 4, 2019 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Hilo ni kosa la nne msimu huu kwa timu ya Yanga kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, na adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Aidha, Yanga pia imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wakati wakirejea vyumbani baada ya mechi dhidi ya Ndanda Fc kumalizika

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu

Beki wake kisiki mkongwe Kelvin Yondani amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Kagera Sugar FC katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 11, 2019 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji

Yondani tayari amekosa mchezo mmoja dhidi ya Mtibwa Sugar