Bodi ya Wakurugenzi klabu ya Simba imemuagiza kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Aussems kuwasilisha ripoti yake kwa ajili ya usajili wa msimu ujao
Simba imedhamiria kuanza mapema maboresho ya kikosi chake ambapo imebainika mikataba ya nyota zaidi ya 10 inamalizika mwishoni mwa msimu
Baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukiongoni ni pamoja na John Bocco, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Paschal Wawa, Paul Bukaba, James Kotei, Asante Kwasi na Nicolas Gyan
Imeelezwa hatma ya wachezaji hao inasubiri mapendekezo ya Aussems ambaye ndiye aliyeachiwa jukumu zima la usajili huku uongozi wa Simba ukibaki katika utekelezaji
Hata hivyo idadi kubwa ya wachezaji hao wataendelea kubaki Msimbazi kutokana na mchango mkubwa waliotoa msimu huu
Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori amesema hawatarajii kukivuruga kikosi chao ambacho kimefanya vizuri msimu huu lakini watasikiliza kile kitakachopendekezwa na Aussems kwa ajili ya maboresho
“Masuala yote ya usajili Simba mwenye kauli ya mwisho ni kocha. Tunafahamu baadhi ya nyota wetu mikataba yao inamalizika, hata hivyo mpaka sasa hakuna mchezaji ambaye kocha amesema tumuache, hivyo tutawapa mikataba mipya,” amesema Magori
Baada ya Simba kuondoshwa hatua ya robo fainali michuano ya Ligi ya Mabingwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ alisema msimu ujao wanataka kuwa na kikosi imara zaidi na hawatasita kuachana na wachezaji ambao mchango wao ni mdogo au watovu wa nidhamu