Dida anolewa kuibeba Simba mchezo dhidi ya Mbao Fc

Mlinda lango namba moja wa Simba Aishi Manula alipata majeraha ya kiganja cha mkono wakati akiitumikia timu ya Taifa kwenye mchezo dhidi ya Uganda

Licha ya kuhudhuria mazoezi ya Simba leo, Manula bado anaonekana hayuko vizuri, ambapo benchi la ufundi limelazimika kumuandaa kikamilifu golikipa namba mbili Deo Munishi ‘Dida’ kuelekea mchezo dhidi ya Mbao Fc

Baada ya mlinda lango kinda Ali Salim kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa U20, Simba imebaki na walinda lango wawili wa kikosi cha kwanza Manula na Dida

Hakuna uhakika kama Manula atakuwa ‘fit’ kabla ya Jumapili lakini huenda Simba ikalazimika kuongeza mlinda lango mwingine kutoka kikosi cha pili kuelekea mchezo wa Jumapili

UWANJA WA SIMBA SC BUNJU

Ujenzi wa uwanja wa Simba ulioko Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es salaam ulisimama kwa muda kutokana na nyasi bandia za uwanja huo kushikiliwa na TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi wa kesi iliyokuwa ikiendelea

Hata hivyo Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori amesema tayari TAKUKURU imeziachia nyasi hizo hivyo wakati wowote ujenzi wa uwanja huo utaendelea

Awali uwanja huo ulitarajiwa kukamilika mwezi wa pili lakini sasa baada ya nyasi hizo kuachiwa, Magori amesema ujenzi utakamilika baada ya wiki mbili

Mwekezaji wa klabu ya Simba Mohammed Dewji ‘Mo’ aliahidi kuukamilisha uwanja huo tayari kuanza kutumika kabla ya msimu huu kumalizika

Michezo ya robo fainali kombe la FA kuanza leo

Michezo ya Robo Fainali kombe la FA (ASFC) inaanza leo ambapo michezo miwili inatarajiwa kupigwa

KMC itakuwa uwanja wa Taifa kuikabili African Lyon wakati Lipuli Fc itakuwa uwanja wa Samora kuikabili Singida United

Keshokutwa Ijumaa, Kagera Sugar itaumana na Azam Fc kwenye dimba la Kaitaba wakati siku ya Jumamosi Yanga itakamilisha michezo ya robo fainali kwa kuivaa Alliance Fc katika mchezo utakaopigwa uwanja wa CCM Kirumba

Zahera atua, kuiongoza Yanga dhidi ya Alliance Fc

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amewasili usiku wa kuamkia leo Jumatano kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na ataungana na kikosi cha Yanga kinachoondoka kesho kuelekea jijini Mwanza

Zahera alikuwa DR Congo kutimiza majukumu ya timu ya Taifa ambapo wamefanikiwa kukata tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019 kama ilivyo kwa Tanzania

Yanga inatarajiwa ‘kukwea pipa’ kesho Alhamisi kuelekea Mwanza tayari kwa mchezo wa robo fainali kombe la Azam (ASFC) dhidi ya Alliance Fc

Mchezo huo utapigwa katika uwanja wa CCM Kirumba, Jumamosi, March 30 2019

AISHI MANULA : MAJERUHI

Mlinda lango namba moja wa Simba na Stars Aishi Manula, huenda akahitaji siku kadhaa za mapumziko baada ya kupata majeraha wakati akiitumikia Taifa Stars kwenye mchezo dhidi ya Uganda juzi

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema Manula hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichofanya maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Mbao Fc Jumapili

Wakati huo huo Aussems amesema wachezaji wote wa Simba waliokuwa na majukumu ya timu za Taifa wanatarajiwa kuanza kuwasili leo kuungana na wenzao ambao walianza mazoezi juzi kwa ajili ya maandalizi ya michezo inayofuata

Ukiondoa Aishi Manula, wachezaji wengine wanaotarajiwa kuripoti kambini kuanzia leo ni John Bocco, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Emmanuel Okwi, Juuko Murshid, Meddie Kagere na Clatous Chama

Ajib, Tuyisenge watajwa Msimbazi

Nahodha wa Yanga Ibrahim Ajib huenda akarejea katika klabu ya Simba, mahali alipokuza jina lake kwenye soka

Inaelezwa Ajib ambaye mkataba wake na Yanga unamalizika mwishoni mwa msimu, tayari amesaini mkataba wa awali kurudi Msimbazi

Ajib alisajiliwa na Yanga mwaka juzi akipishana na Haruna Niyonzima aliyetua Msimbazi

Simba tayari imeanza mkakati wa kukiboresha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao ambapo mbali na Ajib, mabingwa hao wa Tanzania Bara inaelezwa tayari wametua nchini Kenya kumnyakua mshambuliaji wa Gor Mahia, Jacques Tuyisenge

Tuyisenge aliyeisaidia Gor Mahia kutinga robo fainali ya kombe la Shirikisho Barani Afrika, ataondoka Gor Mahia mwishoni mwa msimu mkataba wake utakapokuwa umemalizika

Msimu uliopita Tuyisenge alikuwa pacha wa Meddie Kagere katika kikosi cha Gor Mahia kilichokuwa kikinolewa na Dylan Kerr

Samatta aunga mkono zawadi kwa Kapombe

Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta ameungana na wadau wanaoamini beki Shomari Kapombe ambaye aliumia nchini Afrika Kusini wakati akiwa kambini na kikosi cha Stars, anastahili kupewa zawadi kama walivyopewa wachezaji wote waliyoipeleka Stars fainali za AFCON 2019

Samatta ambaye tayari amerudi Ubelgiji kuungana na KRC Genk, amesema TFF inapaswa kumjumuisha mchezaji huyo kwenye zawadi zinazotolewa kwa kuwa aliumia wakati akitimiza majukumu ya timu ya Taifa

Aidha Samatta amesema kama hilo haliwezekani basi atawashawishi wachezaji wote wagawane na Kapombe kile walichozawadiwa

Samatta amekwenda mbali zaidi kwa kusema kama hilo haliwezekani nalo basi yeye atagawana na Kapombe nusu kwa nusu zawadi alizozawadiwa kama mchezaji wa timu ya Taifa

Nae Kapombe amesema amefurahi uiona Stars inakata tiketi ya kushiriki fainali za AFCON mwaka huu

“Nimefurahi sana kama mtanzania ambaye pia nilikuwa kwenye kikosi huko nyuma licha ya kutolewa baadaye kwakuwa nisingeweza kucheza.

“Natoa pongezi kubwa kwa wachezaji wenzangu, na wale waliosaidia kufika hatua hii.

“Kwakweli ni jambo kubwa sana kutokea kwasababu ni miaka 39 nafasi hii ilikuwa haijatokea kwetu, nina furaha kubwa kwakweli”.

Kapombe amesema hali yake inaendelea vizuri na tayari ameanza mazoezi mepesi akitarajiwa kujiunga na kikosi cha Simba baada ya wiki tatu hadi nne

Tambwe, Makambo, Ngasa wanolewa kuibeba Yanga dhidi ya Alliance FC

Mwishoni mwa wiki hii Yanga inakabiliwa na mchezo muhimu wa robo fainali kombe la Azam (ASFC) dhidi ya Alliance Fc utakaopigwa March 30 kwenye uwanja wa CCM Kirumba

Kocha Msaidizi wa Yanga Noel Mwandila amesema ni lazima wajiandae kikamilifu kuhakikisha wanapata matokeo yatakayo-wapeleka hatua ya nusu fainali

Kocha huyo anayekaimu nafasi ya Zahera, amesema wanaufahamu ubora wa Alliance Fc, kupitia michezo miwili ambayo wamekutana nao kwenye ligi, wanafahamu nini wafanye ili waweze kupata matokeo

“Hatuna cha kupoteza kuelekea mchezo huo tupo makini kila idara tunapambana kuhakikisha tunapata matokeo uwanja wa Kirumba, sio kazi rahisi kwetu kwani tunakutana na wapinzani ambao ni bora kila idara,” Mwadila amenukuliwa na Mwanaspoti

“Wana nguvu, wachezaji vijana na wana kasi tunatarajia kukutana na changamoto kubwa kutoka kwao lakini tumejipanga kukabiliana nazo kwasababu tunatambua umuhimu wa mchezo huo, Ngassa na Makambo wanakasi ya kukimbia na mipira Tambwe atakaa tayari kwaajili ya kumalizia mipira mirefu itakayokuwa inapigwa”

Mwandila ameongeza kuwa hawawezi kucheza mchezo sawa na wapinzani wao wanatarajia kutumia mbinu mbadala ambayo itawasaidia wao kupata matokeo kama ilivyokuwa michezo iliyopita na kuweka wazi kuwa lengo lao ni kupata matokeo mapema ili kuwatoa mchezoni wapinzani wao.

Yanga imekutana mara mbili na Alliance Fc katika michezo ya ligi na Yanga kushinda yote

Kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa Yanga ilishinda mabao 3-0 kabla ya kushinda 1-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa dimba la CCM Kirumba

Itarejea mkoani Mwanza tena katika uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya vijana hao machachari kuwania tiketi muhimu ya kutinga nusu fainali kombe la FA (ASFC)

Baada ya mchezo huo, Yanga itaendelea kutumia dimba la CCM Kirumba kwa michezo yake yote ya nyumbani wakati uwanja wa Taifa utakapokuwa umefungwa kupisha michuano ya kombe la AFCON ya vijana

Simba kwenda Morogoro Ijumaa, kuivaa Mbao Fc Jamhuri Stadium

Mchezo wa ligi kuu kati ya Simba dhidi ya Mbao Fc utapigwa kwenye dimba la Jamhuri Jumapili, March 31 2019 ambapo kikosi cha Simba kinatarajiwa kuelekea mkoani Morogoro Ijumaa ya wiki hii

Meneja wa Simba Patrick Reyemamu amesema wanatarajia kuweka kambi ya mkoani Morogoro kujiandaa na mchezo dhidi ya TP Mazembe

Aidha Simba imechagua kutumia uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya michezo yake ya nyumbani wakati ambao uwanja wa Taifa utakuwa umefungwa kupisha michuano ya AFCON kwa vijana inayoanza April 14-28 2019

Kwa sasa Simba inafanya mazoezi uwanja wa Boko Veterans ambapo wachezaji waliokuwa na majukumu katika timu za Taifa wanatarajiwa kuanza kuwasili kesho