FT : KMC 1-2 Simba

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara, Simba wameendeleza wimbi la ushindi kwenye ligi hiyo baada ya kuichapa KMC mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba

Mshambuliaji Emmanuel Okwi ameendeleza rekodi ya kuzifumania nyavu katika ligi hiyo leo akiitanguliza Simba kwa bao safi alilofunga kwenye dakika ya 23

Okwi amefunga kwenye mchezo wa tatu mfululizo sasa akifikisha mabao 10

KMC iliyokuwa bora katika kipindi cha pili ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Hassani Kabunda kwenye dakika ya 57 kabla nahodha John Bocco hajaihakikishia Simba alama tatu muhimu kwa kuifungia bao la ushindi kupitia mkwaju wa penati katika dakika ya 82

Hiyo ilikuwa penati ya pili kwa Simba kwenye mchezo huo. Meddie Kagere alikosa penati ya kwanza kwenye dakika ya 60

Ushindi huo umeipandisha Simba mpaka nafasi ya pili baada ya kufikisha alama 66 na kuwa sawa na Azam Fc

Hata hivyo Simba ina mtaji mkubwa wa mabao

Sasa zimebaki alama nane tu kuifikia Yanga kileleni, Simba ikihitaji kushinda michezo mitatu tu ili kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi

Kikosi cha Simba kinaelekea mkoani Mara kuikabili Biashara United, mchezo utapigwa keshokutwa Jumamosi, April 27 2019

Kiporo Kimeliwa Simba Waichapa KMC bao 2-1

Hayawi hayawi sasa yamekua ni katika muendelezo wa simba kula viporo ndani ya uwanja wa ccm kirumba mwanza leo timu ya simba ikiibuka na ushindi mnono wa bao mbili kwa moja huku.

Bao la kwanza la Simba limepatikana kutoka kwa Emmanuel Okwi dakika ya 23 na kusawazisha na mchezaji mahiri kabisa kutoka KMC Hassan kabunda mnamo dakika ya 57 baaadae kabisa dakika za lala salama John Bocco ameipatia goli la ushindi kwa mkwaju wa pelnati dakika ya 82.

Ni moja ya mchezo ulio kua na mvutano mkubwa kutoka pande zote mbili huku AK 14 Meddie Kagere akikosa penalt

Kwa matokea haya sasa simba imemfikia azam fc kwa kuwa na point sawa

Simba dimbani leo kuikabili KMC

Kikosi cha Simba leo tena kinashuka katika uwanja wa CCM Kirumba kuikabili KMC kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Baada ya juzi kuichapa Alliance Fc mabao 2-0 kwenye uwanja huo, leo Simba inarejea tena ikiwa na shauku ya kuondoka na alama zote tatu

Kocha Mkuu wa mabingwa hao watetezi Patrick Aussems amesema wanatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa KMC lakini wamejipanga kupata matokeo yatakayowapandisha hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi

Ushindi utaiwezesha Simba kufikisha alama 66 na kuiondoa Azam Fc katika nafasi ya pili kutokana na wingi wa mabao ya kufunga

Katika mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa, Simba ilifanikiwa kuondoka na alama zote tatu kwa ushindi wa mabao 2-1 huku ikifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake

Leo pia Aussems amesema atafanya mabadiliko ya kikosi kwani mchezo wa leo unahitaji uzoefu na ufundi

TMA yatoa tahadhari ujio wa kimbunga Keneth

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetangaza kuwa Kimbunga Kenneth kimeongezeka kasi na kinatarajiwa kufika pwani ya kusini ya Tanzania na kaskazini mwa Msumbiji kuanzia usiku wa leo Alhamisi

Kwa mujibu wa TMA, jana kimbunga hicho kilikuwa kilomita 450 kutoka pwani ya Mtwara na kina kasi ya kilomita 130 kwa saa.

Kimbunga hicho kinatarajiwa kuongeza nguvu zaidi leo Alhamisi mchana ambapo kitakuwa kinasafiri kwa kilomita 170 kwa saa na kitakuwa kilomita 150 kutoka pwani ya Mtwara.

Kwa mujibu wa TMA, eneo husika ambalo kimbunga hicho kitatua litakuwa nchini Msumbiji, kikiwa na kasi ya kilomita 100 kwa saa. Eneo hilo litakuwa kilomita 200 kutoka pwani ya Mtwara.

Hata hivyo, mkoa wa Mtwara na maeneo jirani hususani mikoa ya Lindi na Ruvuma yataathirika pakubwa (athari zinategemewa kufikia umbali mpaka wa kilomita 500 kutoka Mtwara).

TMA imetahadharisha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu na nguvu kubwa (ya upepo na mvua) itakayopelekea madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.

“Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibufu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali. Uharibifu wa mazao mashambani na miundombinu kutokana na mafuriko”

Simba yakamilisha maandalizi ya kuikabili KMC

Kikosi cha Simba leo asubuhi kimefanya mazoezi ya mwisho kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya KMC

Mchezo huo utapigwa kesho Alhamisi kwenye uwanja wa CCM Kirumba

Simba ilishuka katika uwanja huo huo jana kuikabili Alliance Fc katika mchezo ambao Simba ilishinda kwa mabao 2-0

Baada ya mazoezi hayo yaliyosimamiwa na kocha Patrick Aussems, wachezaji walipewa mapumziko kusubiri mchezo huo wa kesho

Ratiba ya mabingwa hao watetezi haitoi nafasi kwa wachezaji kupata mapumziko ya kutosha hivyo benchi la ufundi kulazimika kupunguza muda wa mazoezi ili kuwapumzisha wachezaji

Hii hapa ‘bandika-bandua’ ya michezo ya Simba

Ratiba imebana kwelikweli! Ndio kauli unayoweza kuitumia kwa Simba ambayo imekuwa ikishuka dimbani kila baada ya siku mbili au siku tatu

Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Alliance Fc jana, kesho Simba itashuka tena uwanja wa CCM Kirumba kuikabili KMC katika mchezo mwingine wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Kocha Mkuu wa mabingwa hao watetezi Patrick Aussems amesema ataendelea kufanya ‘rotation’ ya kikosi chake ili kuhakikisha wanafikia malengo ya kutetea ubingwa

Hii hapa ratiba ya Simba kwa michezo iliyobaki mpaka mwishoni mwa msimu;
25/04/19 KMC Vs Simba SC .
27/04/19 Biashara Utd FC Vs Simba Sc.

30/04/19 Simba Sc Vs JKT Tanzania .
03/05/19 Mbeya City FC Vs Simba Sc.
06/05/19 Tanzania Prisons FC Vs Simba SC.

08/05/19 Simba SC Vs Coastal Union.
10/05/19 Simba SC Vs Kagera sugar FC.

13/05/19 Simba SC Vs Azam FC.
16/05/19 Simba SC Vs Mtibwa Sugar FC.

19/05/19 Simba SC Vs Ndanda FC.
22/05/19 Singida United vs Simba Sc.

25/05/19 Simba SC Vs Biashara United.

28/05/19 Mtibwa Sugar FC Vs Simba SC.

Ushindi dhidi ya Alliance umetuongezea morali – Niyonzima

Kiungo Haruna Niyinzima amesema ushindi wa mabao 2-0 waliopata jana dhidi ya Alliance Fc umewaongezea morali wachezaji na wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanatetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Niyonzima aliye katika kiwango bora, aliifungia Simba bao la kwanza na baadae Okwi kuongeza la pili katika kipindi cha pili

“Mchezo haukuwa rahisi hasa kutokana na matokeo tuliyopata kwenye mchezo uliopita, tulikuwa na presha ya kupata ushindi,” amesema Niyonzima

“Tunashukuru tumefanikiwa kuondoka na alama zote tatu, matokeo haya yametuongezea morali ya kufanya vizuri kwenye michezo ijayo”

Akizungumzia ugumu wa ratiba, Niyonzima amesema Simba ilisajili wachezaji 30 hivyo anaamini wataweza kukabiliana na changamoto ya kucheza kila baada ya siku mbili au tatu

“Kocha alituambia atakuwa akifanya mabadiliko ya kikosi ili kuhakikisha kila mchezaji anahusika. Hii ndio faida ya kusajili wachezaji wengi”

“Najua haitakuwa kazi rahisi lakini naamini tutafanikiwa kutetea ubingwa”

Simba imebaki jijini Mwanza ambapo kesho itashuka tena kwenye uwanja wa CCM Kirumba kuikabili KMC

Djuma yamkuta Rwanda, atimuliwa As Kigali

Aliyewahi kuwa kocha Msaidizi wa Simba Masudi Djuma ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo, ametimuliwa klabu ya AS Kigali aliyokuwa akiifundisha

Djuma alijiunga na AS Kigali mwezi Oktoba mwaka jana baada ya uongozi wa Simba kuvunja mkataba wake akituhumiwa kumfanyia hujuma kocha Patrick Aussems

Djuma ameinoa AS KIgali kwa muda wa miezi saba tu akitimuliwa baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo mitano iliyopita bila ya kupata ushindi

FT : Alliance 0-2 Simba

Simba imeendeleza mawindo yake ya ubingwa wa pili mfululizo ambapo leo imefanikiwa kuibomoa Alliance Fc mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba

Simba iliyokuwa na mabadiliko katika kikosi kilichoanza, ilijipatia bao la kuongoza kwenye dakika ya 21 kupitia kwa kiungo fundi Haruna Niyonzima

Bao la pili liliwekwa kambani na Emmanuel Okwi kwenye dakika ya 75

Okwi alianzia benchi kwenye mchezo huo ambapo aliingia katika dakika ya 64 kuchukua nafasi ya Adam Salamba

Hilo lilikuwa bao la tisa kwa Okwi msimu huu sasa akiwa amefunga katika michezo yote miwili iliyopita

Matokeo hayo yameifanya Simba ifikishe alama 63 sasa ikiwa nyuma ya Azam Fc kwa tofauti ya alama tatu

Ushindi katika mchezo unaofuata dhidi ya KMC utaipaisha Simba hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi

Simba itaendelea kubaki jijini Mwanza kusubiri mchezo dhidi ya KMC ambao utapigwa keshokutwa Alhamisi, katika uwanja wa CCM Kirumba