Tunahitaji ushindi dhidi ya Alliance Fc – Mkude

Kiungo Jonas Mkude amesema wanafahamu hawana nafasi ya kufanya makosa zaidi kwani wanahitaji kutetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Simba iko mkoani Mwanza ambapo leo itachuana na Alliance Fc katika mchezo utakaopigwa uwanja wa CCM Kirumba

Akizungumza baada ya mazoezi ya jana jioni, Mkude alisema baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar, wanahitaji kupata matokeo dhidi ya Alliance Fc leo

“Hakuna mechi rahisi katika Ligi Kuu, lakini timu itakayokuwa na nidhamu uwanjani ndiyo yenye asilimia kubwa ya kupata pointi tatu muhimu. Tunahitaji kuwa kwenye ubora wetu ili tuweze kushinda kesho (leo)” amesema

Aidha, Mkude alisema hakuna timu inayoingia uwanjani kwa ajili ya kufungwa, ila anayeruhusu kufanya makosa ndiyo yanaweza kuwagharimu na hatimaye kupoteza mchezo.

“Tumekuja kupambana, mechi zetu hizi zimekuwa zinatizamwa sana na wapinzani wetu, tukifanya vizuri itatusaidia kutetea ubingwa tunaoushikilia na hiyo ndiyo mipango yetu”

Baada ya mechi ya leo, Simba itaendelea kubaki jijini Mwanza kusubiri mchezo dhidi ya KMC FC utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba pia.

Simba yapania kufuta makosa CCM Kirumba leo

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo wanashuka kwenye uwanja wa CCM Kirumba kuikabili Alliance Fc katika mchezo unaotarajiwa kupigwa saa kumi kamili jioni

Kikosi cha Simba kiko jijini Mwanza tangu juzi kikiendelea na maandalizi ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka

Baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar, Simba imepania kusahihisha makosa yake na kuibuka na ushindi dhidi ya Alliance Fc leo

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema anafahamu mchezo hautakuwa mwepesi lakini wanahitaji kuondoka na alama zote tatu

Katika mchezo wa leo Simba itamkosa beki kiraka Erasto Nyoni ambaye ni mgonjwa

Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amewataja Nyoni, Paschal Wawa na Shomari Kapombe kuwa wachezaji pekee watakaokosekana kwenye mchezo huo

Simba iliyoshuka dimbani mara 24 inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia alama 60

Bado mabingwa hao watetezi wana michezo nane ya viporo ambayo kama watashinda yote watajikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama 10 dhidi ya Yanga inayoongoza

Nyoni augua ghafla, kuikosa Alliance Fc

Simba imepata pigo baada ya beki kiraka Erasto Nyoni kuugua ghafla hivyo atakosa mchezo wa kesho dhidi ya Alliance Fc

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amethibitisha kuwa Nyoni hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachoshuka dimbani kuikabili Alliance Fc

Nyoni anaungana na beki Paschal Wawa ambaye hakusafiri jijini Mwanza kutokana na majeruhi yanayomkabili

Simba yajifua CCM Kirumba, kamili kuikabili Alliance Fc

Kikosi cha Simba leo jioni kimefanya mazoezi kwenye uwanja wa CCM Kirumba yakiwa ni maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Alliance Fc

Mchezo huo utapigwa kesho Jumanne, April 23 katika uwanja huo

Simba ilitua Mwanza mapema jana ikitokea Kagera ambako ilipoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar kwa kuchapwa mabao 2-1

Katika mazoezi hayo yaliyosimamiwa na kocha Patrick Aussems, Simba iliwaruhusu kukaa jukwaani mashabiki waliofika kuwashuhudia mabingwa hao watetezi

Kuelekea mchezo huo, Aussems amesema wanatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa Alliance Fc kutokana na ubora wa kikosi cha timu hiyo

Hata hivyo amesema Simba inahitaji kushinda mchezo huo hasa baada ya kupoteza mchezo uliopita

“Tunajua haitakuwa mechi rahisi sababu Alliance ni timu nzuri lakini sisi tumepoteza mchezo Bukoba na kesho tunataka alama tatu,” amesema Aussems

“Tunajua kwanini tulipoteza na tumejiandaa kwa hilo na ninaamini kesho tutakuwa vizuri.”

Simba Queens yaifumua Yanga Princess 5-1

Wanamama wa Simba Queens leo wameendeleza ubabe kwa watani zao Yanga Princess baada ya kuwafumua mabao 5-1 katika mchezo wa ligi kuu ya Wanawake, Serengeti Lite uliopigwa uwanja wa Karume

Magoli ya Simba Queens yalipachikwa na Opah Clement aliyefunga mabao mawili, Mwanahamisi Omary, Joele Bukulu na Amina Ramadhani na goli pekee la Yanga Princess likifungwa na Fausta Thomas

Huu ni ushindi wa pili kwa Simba Queens dhidi ya watani zao, wakipata ushindi wa mabao 7-0 katika mchezo wa duru ya kwanza wa ligi hiyo ya Wanawake

Nyota kibao Simba kumaliza mikataba mwishoni mwa msimu

Bodi ya Wakurugenzi klabu ya Simba imemuagiza kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Aussems kuwasilisha ripoti yake kwa ajili ya usajili wa msimu ujao

Simba imedhamiria kuanza mapema maboresho ya kikosi chake ambapo imebainika mikataba ya nyota zaidi ya 10 inamalizika mwishoni mwa msimu

Baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukiongoni ni pamoja na John Bocco, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Paschal Wawa, Paul Bukaba, James Kotei, Asante Kwasi na Nicolas Gyan

Imeelezwa hatma ya wachezaji hao inasubiri mapendekezo ya Aussems ambaye ndiye aliyeachiwa jukumu zima la usajili huku uongozi wa Simba ukibaki katika utekelezaji

Hata hivyo idadi kubwa ya wachezaji hao wataendelea kubaki Msimbazi kutokana na mchango mkubwa waliotoa msimu huu

Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori amesema hawatarajii kukivuruga kikosi chao ambacho kimefanya vizuri msimu huu lakini watasikiliza kile kitakachopendekezwa na Aussems kwa ajili ya maboresho

“Masuala yote ya usajili Simba mwenye kauli ya mwisho ni kocha. Tunafahamu baadhi ya nyota wetu mikataba yao inamalizika, hata hivyo mpaka sasa hakuna mchezaji ambaye kocha amesema tumuache, hivyo tutawapa mikataba mipya,” amesema Magori

Baada ya Simba kuondoshwa hatua ya robo fainali michuano ya Ligi ya Mabingwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ alisema msimu ujao wanataka kuwa na kikosi imara zaidi na hawatasita kuachana na wachezaji ambao mchango wao ni mdogo au watovu wa nidhamu

Simba Queens yaiandalia kipigo Yanga Princess leo

Wakinadada wa Simba Queens leo watashuka kwenye uwanja wa Karume kupepetana na watani zao wa jadi Yanga Princess katika mchezo wa ligi kuu ya Wanawake, Serengeti Lite

Simba Queens inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo, imepania kuendeleza umwamba dhidi ya wapinzani wao hao ambao wanashika nafasi ya saba

Katika mchezo wa raundi ya kwanza Simba Queens iliibamiza Yanga Princess mabao 7-0

JKT Queens inaongoza ligi ikiwa imejikusanyia alama 45 ikiwa imeshinda michezo yake yote.

Mlandizi Queens inashika nafasi ya pili ikiwa imejikusanyia alama 32 sawa na Alliance Girls timu hizo zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa

Simba Queens iko nafasi ya nne ikiwa na alama 31 wakati Yanga Princess inashika nafasi ya saba ikiwa na alama 19

Aussems ameipaisha Simba, asubiri kusaini mkataba mpya

Wakati alipokabidhiwajukumu la kuinoa Simba mwanzoni mwa msimu, Patrick Aussems alipewa masharti mawili; moja ni kuipeleka Simba hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika na pili ni kutetea ubingwa ligi kuu

Aussems amekamilisha sharti la kwanza na kuvuka malengo baada ya kufanikiwa kuivusha Simba hadi robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa

Sharti lililobaki ni la kutetea ubingwa wa ligi kuu, sharti ambalo nalo anaelekea kulikamilisha

Mbelgiji huyo aliyechukua nafasi ya Pierre Lechantre, hakuna shaka atapewa mkataba mpya kuendelea kuinoa Simba kutokana na mafanikio aliyoipatia timu hiyo msimu huu

Mkataba wake na Simba aliosaini msimu uliopatita utamalizika mwishoni mwa msimu

Simba ilivyojifua Mwanza

Baada ya kuwasili jijini Mwanza mapema leo, jioni kikosi cha Simba kiliendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Alliance Fc

Mchezo huo utapigwa keshokutwa, April 23 2019 katika uwanja wa CCM Kirumba