Baada ya kufungwa bao 1-0 msimu uliopita kwenye uwanja wa CCM Kambarage, Leo Yanga inashuka tena katika uwanja huo kusaka alama tatu muhimu.
Changamoto zilizoikumba Yanga mwishoni mwa msimu uliopita zilipelekea kupoteza mchezo dhidi ya Mwadui Fc uliopigwa May 19 2018 ukiwa ni mchezo wa tatu Yanga kufungwa mfululizo baada ya pia kufungwa na Prisons na Mtibwa Sugar.
Wakati huo Yanga ilikwenda Shinyanga ikiwa na wachezaji 13 tu wa kikosi cha kwanza kilichoongozwa na aliyekuwa kocha msaidizi Shedrack Nsajigwa.
Lakini hali ni tofauti msimu huu ambapo Yanga iko mkoani humo ikiwa na kikosi chake kamili sambamba na kocha wake Mwinyi Zahera
Ni mchezo ambao Yanga inahitaji kuibuka na ushindi ili kulinda rekodi yake ya kutofungwa lakini pia kujiimarisha katika mbio za kuwania ubingwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa timu za Azam Fc na Simba
Tangu kuanza kwa msimu wa 2018/19 Yanga haijapoteza mchezo wowote katika ligi na hata michezo ya kirafiki.
Kikosi hicho cha Zahera kimeweka rekodi ya kipekee kikiwa kimecheza karibu miezi mitatu bila ya kufungwa kinyume na matarajio ya wale waliokuwa wakibeza.
Mara ya mwisho Yanga kufungwa ilikuwa August 28 kwenye mchezo wa mwisho wa kombe la shirikisho hatua ya makundi dhidi ya Rayon Sport nchini Rwanda ambapo Yanga ilifungwa bao 1-0
Yanga imecheza michezo 10 kwenye ligi bila ya kupoteza ikishinda michezo nane na kutoka sare michezo miwili.
Inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 26 sawa Simba lakini Yanga ikiwa imecheza michezo pungufu
Category: yanga
Kabwili,Ninja Kuongeza Nguvu Shinyanga | Yanga vs Mwadui
Mlinda lango Ramadhani Kabwili, walinzi Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Godfrey Paulo ‘Boxer’ wametua mkoani Shinyanga kuongeza nguvu kwenye kikosi cha Yanga kinachoshuka uwanja wa CCM Kambarage leo kuumana na Mwadui FC.
Wachezaji hao walikuwa kwenye timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 23 ambayo juzi iliondoshwa kwenye michuano ya kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019 kwa ngazi ya vijana licha ya kushinda kwa mabao 3-1 dhidi ya Burundi baada ya kufungwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza.
Kuwasili kwa wachezaji hao, kumeongeza nguvu kwenye kikosi cha Yanga ambacho kitawakosa nahodha Kelvin Yondani na mlinda lango Beno Kakolanya ambao hawakusafiri kwa sababu binafsi.
Yanga imedhamiria kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo ili kuendeza rekodi ya kutofungwa msimu huu pia kuendeleza presha kwa wapinzani wake katika mbio za ubingwa, Azam fc na Simba
UCHAGUZI: Yanga yarudi BMT kusaka Suluhu
Uongozi wa Yanga umeliomba Baraza la Michezo la Taifa (BMT) liingilie kati kumaliza mvutano uliopo kati ya TFF na Yanga kuhusu uchaguzi wa kujaza nafasi zilizowazi utakaofanyika Januari 13 2019.
Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi zilizotangazwa lilifungwa rasmi jana Jumatatu saa 10:00 jioni lakini uongozi wa Yanga umeendelea na msimamo wake wa kupinga uchaguzi kwa nafasi ya Mwenyekiti.
Yanga pia haikubaliani na uchaguzi wake kusimamiwa na TFF.
Taarifa iliyopatikana jana ilieleza kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameunga mkono uamuzi wa Yanga kwenda BMT kusaka suluhu kwani anaamini Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga anaweza kumaliza utata huo.
“Nimesikia upande mmoja unataka kwenda BMT nimefurahi sana waende wakae chini ya mwanasoka mzoefu Tenga (Leodegar) awasikilize pande zote mbili kuna shida gani ikishindikana pale litakuja kwangu,”Dk Mwakyembe amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti.
“Mimi naamini hili ni suala la kutumia busara tu, sioni kama ni gumu halina ugumu wowote wanachoshindana ni mambo mawili kwanza wanataka kamati yao ya uchaguzi ndio isimamie uchaguzi na TFF wanasema mbona hamtoshi, ni mvutano huo sasa tutaangalia kama wanaweza au kama hawawezi tutafanya maamuzi.
“Pili ni kuhusu Yusuf Manji hakuna anayekataa kwamba Wanayanga wanampenda sana, lakini katika nchi kuna kanuni na sheria hata kama unampenda, we mpende nyumbani kwako unapokuwa kwenye nchi kuna sheria, lazima tuangalie kuna kitu gani Yanga wanataka na sheria pia,” aliongeza Dk Mwakyembe
Pia wakati Yanga ilipokwenda Ruangwa kucheza na Namungo kwenye mchezo wa kirafiki, viongozi wa timu hiyo walimuomba Waziri Mkuu Mh Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mchezo huo kuingilia kati kupata suluhu ya mgogoro huo
USAJILI: Yanga kushusha Kifaa Hiki Kutoka UGANDA
Taarifa za uhakika ni kwamba Yanga imekamilisha mazungumzo na mshambuliaji wa Kimataifa wa Uganda Nelson Senkatuka anayechezea Bright Stars inayoshiriki ligi kuu nchini humo.
Senkatuka anatarajiwa kutua nchini wiki ijayo ili kukamilisha taratibu za usajili tayari kuanza kuwatumikia mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania.
Msimu uliopita Senkatuka aliifungia Brights Stars mabao 18 kwenye ligi kuu ya Uganda.
Mabosi wa Kamati ya usajili ya Yanga wako ‘busy’ kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili kuhakikisha wanaongeza nguvu kwenye kikosi cha timu hiyo ambacho kinashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi
TFF: Hatumtambui MANJI lazima Uchaguzi Ufanyike
Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF mchana huu limesema kuwa hawatambui kurejea kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga Sc Yusuph Manji hivyo uchaguzi utafanyika kama kawaida. .
.
Aidha shirikisho hilo limesisitiza mbele ya waandishi wa habari kuwa zoezi la kuchukua fomu kwaajili ya wagombea wanaowania nafasi zilizowazi ndani ya klabu hiyo linaendelea hivyo kama wanayanga wanamtaka Manji basi achukue fomu na kama wana Yanga wanamtaka basi atapita bila wasiwasi ila cha msingi uchaguzi kufanyika. .
.
Mbali na hilo TFF wamefika mbali zaidi na kusema wamepata taarifa za mkutano wa dharura wa Yanga wanaotarajia kuufanya November 24 na kuhudhuriwa na Yusuph manji, hivyo Manji anatakiwa kuhudhuria kama mwanachama wa Yanga na si kama Mwenyekiti kwani wao wanatambua nafasi ya Mwenyekiti ndani ya Yanga Sc iko wazi.
.
.
Katika hatua nyingine shirikisho hilo limesema litakuwa tayari kushirikiana na kamati ya uchaguzi ya Yanga Sc kusimamia zoezi zima la uchaguzi na si kuwaachia kama wao wanavyotaka kwakuwa walishapata barua kadhaa kutoka TFF kuwataka wafanye uchaguzi lakini hawakufanya, hivyo ni wakati wa TFF kusimamia suala hilo.
#sokaonlineUpdates
Yanga: zoezi la utolewaji Fomu
Zoezi la utolewaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa Yanga linatarajiwa kufungwa leo Jumatano, Novemba 14 2018 ambapo mpaka sasa watu 12 wamejitokeza kuchukua fomu.
Licha ya uongozi wa Yanga kusisitiza kuendelea kumtambua Mwenyekiti Yusufu Manji, Shirikisho la soka Tanzania (TFF) limesema haliyatambui maamuzi hayo na limeendelea na mchakato wa uchaguzi utakaohusisha nafasi hiyo ya Mwenyekiti.
Jana TFF imewafungia kutojihusiaha na soka nchini kwa miaka mitatu viongozi wa Matawi Yanga, Mwenyekiti Bakili Makele na Katibu Boaz Ikupilika baada ya kuwapata na hatia ya kupinga mchakato wa uchaguzi unaoendelea
Mpaka sasa aliyejitokeza kuwania Uwenyekiti wa Yanga ni Jonas Tiboroha, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga.
Yono Kevela yeye amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Waliochukua fomu kuwania nafasi nne za Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Hamad Ally, Benjamin Jackson, Silvestoer Haule, Musa Katabaro, Said Baraka, Pindu Luhoyo, Dominic Francis na Jeko Jihadhari.
Yanga vs Reha Fc Leo Nov 14
Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania, Yanga leo wanashuka kwenye uwanja wa Uhuru kuikabili Reha Fc katika mchezo wa kirafiki kwa ajili ya kukiandaa kikosi hicho.
Huo unakuwa mchezo wa pili kwa Yanga kipindi hiki ambacho ligi imesimama kupisha michuano ya Kimataifa. Jumapili iliyopita iliilaza African Lyon bao 1-0.
Ni kwa Tsh 5,000/- tu utaushuhudia mchezo huo ukiwa umekaa majukwaa ya VIP wakati kule upande wa mzunguuko ni Tsh 3,000/-
MANJI Kuhudhuria Mkutano Mkuu Nov 24
Siku moja baada ya kutangazwa rasmi kurejea kwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, Baraza la Wadhamini limeridhia kufanyika kwa mkutano mkuu wa dharura lakini habari zaidi zinasema Manji atahudhuria mkutano huo wa kwanza.
Kamati ya utendaji ya Yanga juzi iliagizwa na Baraza la Wadhamini kuandaa mkutano mkuu na haraka utekelezaji wake umefanyika.
Jana jioni Baraza la Wadhamini la Yanga limeridhia kufanyika kwa mkutano mkuu wa dharura utakaofanyika Novemba 24.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema Baraza la Wadhamini ambalo jana pia lilikutana kwa ukamilifu liliridhia mkutano huo.
Taarifa zaidi zinasema katika mkutano huo, Manji amekubali kushiriki katika mkutano huo ambao kama atafika basi utakuwa mkutano wake wa kwanza tangu atangaze kujiuzulu.
“Tumefanya mkutano na kukubaliana ni bora tufanye mkutano wa dharura ili tuweze kuwekana sawa na mikutano kama hii ndiyo muhimu kutuunganisha,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji.
“Tunataraji pia mwenyekiti wetu Manji amethibitisha kuhudhuria, wanaotaka kusikia kauli yake basi wajiandae kumsikia siku hiyo.”
KOCHA Yanga + Wachezaji Wafurahia kurejea kwa MANJI
Achana na shangwe la wachezaji wa Yanga baada ya kusikia Mwenyekiti wao, Yusuf Manji amerejea katika nafasi yake, Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mwinyi Zahera ghafla tu amefunguka akisema taarifa hizo zilizomshtua kisha akasema, kama mkubwa amerudi basi ubingwa Yanga ni mali yao.
Pia, Zahera amesema mkakati wake wa kusajili mastaa watatu wa maana ndani ya kikosi chake, umepata mzuka kwani, anaamini mabosi wa Kamati ya Usajili ikiongozwa na Hussen Nyika, watamkabidhi majina hayo.
Akizungumza na Mwanaspotikutoka kwao DR Congo Zahera amesema kurejea kwa Manji na kama mambo yatatulia baada ya kurudi kwake, basi Yanga haiwezi kupishana na ubingwa msimu huu.
Alisema kila walipokuwa wakikutana na wakati mgumu katika timu yao walikuwa wanakumbushana kumwombea Manji ili mambo yakae sawa na arejee ili arudi klabuni.
Kocha huyo alisema kurejea kwa Manji kisha Yanga ikafanya usajili aliokusudia kuufanya, hakuna namna timu yake inaweza kuukosa ubingwa msimu huu.
Amesisitiza kuwa akirejea ataliamsha kwa wachezaji wake kwa kuwataka kufanya kazi kwa nguvu zaidi kwani sasa matatizo yao yatashughulikiwa na uongozi na wao wanatakiwa kuchapa kazi.
“Nimeshtuka sana kusikia hizo taarifa, niliacha hata kula, nimefurahi sana hii ni habari njema kwangu na kwa Wanayanga wote wanaotaka mafanikio ya hii timu,” alisema Zahera.
“Hamjui kila wakati tulikuwa tunaambiana kwenye timu tuzidishe maombi tumwombee kiongozi wetu Manji arudi kila mchezaji na wasaidizi wangu wanajua nguvu ya bosi wetu.
“Nasema kama Manji amerudi halafu tukafanya usajili wa wachezaji watatu ambao, nataka kufanya kwenye dirisha dogo, sioni nani anaweza kuizuia Yanga isiwe bingwa.
“Tusubiri kuona lakini nikirudi wachezaji wangu wajiandae nataka tufanye kazi ya nguvu kuliko iliyofanyika nyuma ili tumrudishe kwa mafanikio kiongozi wetu, najua matatizo yao sasa yatashughulikiwa.
Wachezaji nao walipuka
Kule nchini Afrika Kusini walipo baadhi ya wachezaji wa Yanga katika kambi ya kikosi cha Taifa Stars ongeza na wale waliobaki nchini wamelipuka kwa furaha wakisema ‘bosi karudi’.
Kiungo Feisal Salum “Fei Toto alisema bado haamini licha ya kuona vipande vya video na picha juu ya kurejea kwa Manji.
“Mpaka sasa siamini hizo taarifa naona picha na video lakini nikimwona nitaamini zaidi hii ni habari njema kwetu,” alisema Fei Toto.
Naye beki Andrew Vincent “Dante alisema wamepokea kwa faraja taarifa hizo na sasa wanasubiri kutangaziwa rasmi na viongozi wao.
“Kusema kweli hakuna ambaye anaweza kusikia taarifa za Manji karudi alafu akanuna labda awe sio mtu anayetaka mafanikio ngoja tusubiri viongozi waje watutangazie kwanza,” alisema Dante











