Beki kisiki wa Simba Paschal Serge Wawa ataukosa mchezo wa pili wa robo fainali ligi ya mabingwa dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa Jumamosi, April 13 huko Lubumbashi DR Congo
Wawa alipata majeraha ya kifundo cha mguu kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa ambao ulimalizika kwa suluhu ya bila kufungana
Uongozi wa Simba umethibitisha kuwa Wawa atakaa nje kwa wiki moja
Wawa hatajumuishwa kwenye kikosi cha Simba kitakachoondoka Alfajiri ya kesho kuelekea Lubumbashi
Game za mzunguuko wa kwanza wa robo fainali ya UEFA Champions League zimechezwa jana nchini England, usiku wa April 9 zimechezwa game mbili ambazo zilikuwa zinakutanisha timu tatu za England, Man City alikuwa ugenini kucheza dhidi ya Tottenham wakati Liverpool alikuwa nyumbani Anfield kuikaribisha FC Porto ya Ureno.
Mchezo wa Man City dhidi ya Tottenham ulimalizika kwa Tottenham kupata ushindi wa goli 1-0 lililofungwa na Heung-Min Son dakika ya 78, wakati Liverpool nao wakiilaza FC Porto kwa magoli 2-0 yaliofungwa na Naby Keita dakika 5 na Firmino dakika ya 26 ya mchezo.
England ambao ndio wanakutanisha timu nyingi katika hatua hii ya robo fainali wakiingiza jumla ya timu nne (Tottenham, Liverpool, Man City na Man United) watalazimika kuziombea dua timu zao hili zifanye vizuri katika hatua hiyo japo moja italazimika kuishia hatua ya robo fainali 100% (Man City na Tottenham) kwa kukutana wenyewe kwa wenyewe, mechi za April 10 ni Man United dhidi ya FC Barcelona na Ajax dhidi ya Juventus.
Timu yetu ya vijana kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Taifa ya Cameroon U-17, mchezo huo utachezwa kesho kwenye viwanja vya JK Youth Park kuanzia saa 9:30 alasiri. #NguvuMoja
Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, amesema kuwa katika historia yake ya kufundisha soka, hajawahi kushindwa baada ya kutinga robo fainali.
Aussems ambaye msimu huu amevuka malengo kwa kuipeleka Simba robo fainali, amesema baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya TP Mazmebe kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana, anaamini mchezo wa marudiano utakaopigwa April 13 Simba ina nafasi ya kushinda kama ilivyo kwa wapinzani wao TP Mazembe
“Katika historia yangu ya soka na timu ambazo nimewahi kufundisha, nilizivusha hatua ya robo fainali, ndio maana sina hofu na hili kwa uwezo wa Mungu tutafanikiwa,” amesema.
Aussems amesema anatambua ni makosa madogo waliyoyafanya katika mchezo wa kwanza na kwamba amejipanga kikamilifu kukabiliana na mchezo huo.
“Natambua kuwa Watanzania na mashabiki wa Simba walikuwa na hofu pengine tungefungwa mabao mengi na TP Mazembe katika mchezo uliopita, lakini wameshuhudia namna tulivyopambana, sidhani kama tunaweza kushindwa mchezo wa marudiano.
“Pengine hofu kubwa ni kwa sababu tutakuwa ugenini, mimi naamini kuwa mpira ni dakika 90, hata tuwe wapi ni plani yangu na juhudi za wachezaji ndizo zitakazoleta matokeo mazuri,” alisema Aussems.
Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere, amewaondoa wasiwasi mashabiki wa Simba kuwa waiamini timu yao kwani kupata ushindi Lubumbashi, Congo inawezekana.
Jumamosi, Simba ililazimishwa suluhu ya ila kufungana dhidi ya TP Mazembe, kwenye mchezo wao wa robo fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar res Salaam.
Matokeo hayo yanailazimu Simba kupata ushindi au sare yoyote ya mabao ugenini ili iweze kutinga nusu fainali
Mchezo wa marudiano utapigwa Aprili 13, nchini Congo kwenye Uwanja wa TP Mazembe.
Kagere alisema anaamini kwa juhudi walizonazo, bado wana nafasi ya kushinda mchezo wao huo.
Alisema kiwango chao si kibaya na hata juzi walicheza vizuri, wakienda ugenini hata kama watatoka sare haitakuwa mbaya.
“Mazembe ni timu kubwa na tulicheza vizuri ila tulikosa bahati ya kupata mabao, tayari tunawajua vizuri hivyo tutacheza zaidi ya tulivyopambana nyumbani, mashabiki wasikate tamaa,” Kagere amenukuliwa naBingwa
Simba inatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam Alfajiri ya Alhamisi kuelekea nchini Congo tayari kwa mchezo huo
Ligi Kuu ya Tanzania Bara inamalizika mwezi ujao na tayari michakato ya usajili wa wachezaji imeanza kushika kasi
Nyota nane wa kikosi cha Simba mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu ambapo Mwenyekiti wa Simba Swedy Mkwabi amesema wako mbioni kuanza mazungumzo ya kuhuisha mikataba ya wachezaji hao
Miongoni mwa nyota ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu ni pamoja na Emmanuel Okwi, John Bocco, Jonas Mkude, Aishi Manula, Erasto Nyoni, James Kotei, Asante Kwasi na Shomari Kapombe
“Tunasubiri ripoti ya Mwalimu Aussems ili tuanze michakato ya usajili. Lakini bila shaka, wachezaji wengi tutaendelea nao” amesema
“Hakuna mchezaji yeyote ambaye mkataba wake wa kuitumikia Simba utakuwa umemalizika na tumempa ruhusa ya kuondoka kwa maana ya kwenda kujiunga na timu nyingine wote tuna mipango nao na tunaimani watasaini mikata mipya ya kubaki hapa.
“Bodi bado haijazungumza na mchezaji yeyote, ambaye mkataba wake unamalizika kutokana na majukumu ya mechi za kimataifa ambazo tunacheza mfululizo, lakini nadhani tutakaa nao na mambo yatakwenda sawa kwa pande zote mbili tutakubaliana”
Mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Simba dhidi ya Biashara United uliokuwa upigwe leo katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, umeahirishwa ili kuipa nafasi Simba kujiandaa na mchezo dhidi ya TP Mazembe
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura amesema mchezo huo umeahirishwa kutokana na Simba kukabiliwa na mchezo huo muhimu wa marudiano robo fainali ya ligi ya mabingwa
Simba sasa itachuana na Biashara baada ya kumalizana na TP Mazembe April 13 2019
Wekundu wa Msimbazi wameendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Boko Veterans kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa Lubumbashi, DR Congo