Nyoni awaita mashabiki uwanja wa Taifa

Kiraka Erasto Nyoni amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa keshokutwa katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS Vita Club

Nyoni aliyerejea kikamilifu baada ya kupona majeraha, amesema upande wao wachezaji wanajifua kikamilifu ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo

“Mchezo huu ni fainali kwetu, tunahitaji kushinda ili tuweze kutinga robo fainali. Mawazo yetu yote yako katika mchezo huo,” amesema

“Tunahitaji sana sapoti ya mashabiki wetu. Tunajua wakija kwa wingi wataongeza hamasa kwetu na kutuongezea ari ya kupambana”

Kikosi cha Simba chini ya kocha Patrick Aussems na Msaidizi wake Denis Kitambi leo kimejifua kwenye uwanja wa Taifa ikiwa ni maandalizi yake ya mwisho kwenye uwanja huo kabla ya mchezo keshokutwa

Wapinzani wao AS Vital Club waliwasili jijini Dar es salaam jana ambapo leo wamefanya mazoezi katika viwanja vya Ghymkhana

Timu hiyo itajifua kwenye uwanja wa Taifa kesho

Mzee Akilimali augua Bagamoyo

Hali ya Mwanachama maarufu wa klabu ya Yanga Mzee Ibrahim Akilimali inaelezwa sio nzuri ambapo amelazwa Hospitali ya Baobab akiendelea na matibabu ya ugonjwa kisukari

Mzee Akilimali amewaomba wadau wa Yanga na Watanzania wote kwa ujumla wamuombee ili aweze kupona maradhi yanayomsumbua

“Hali yangu sio nzuri. Niko huku Bagamoyo najiuguza maradhi ya kisukari. Mniombee kwani kisukari kinanitesa sana,” Mzee Akilimali amenukuliwa na Spoti Xtra

Mzee Akilimali ni miongoni mwa wanachama wa Yanga vinara wa kutoa maoni juu ya masuala mbalimbali ya klabu hiyo

Wakati mwingine hujikuta akiingia katika mgogoro na wanachama wenzake, wakimtuhumu kuwa ni mpinga maendeleo.

Ajib mgonjwa, kuikosa Lipuli Fc

Nahodha wa Yanga Ibrahim Ajib ameondolewa katika kikosi kinachosafiri kwenda mkoani Iringa baada ya kuugua

Yanga itaikabili Lipuli Fc bila ya kuwa na mpishi wake huyo wa mabao aliyehusika katika mabao 21 kati ya 45 yaliyofungwa kwenye ligi

Hata hivyo kukosekana kwake hakuwezi kuwa tatizo kwa kikosi cha Mwinyi Zahera kilichosheheni viungo wengi

Mohammed Issa ‘Banka’, Thabani Kamusoko na Haruna Moshi ‘Boban’ wote wanaweza kucheza nafasi yake.

Kwa michezo ya hivi karibuni, Ajib amekuwa akitokea benchi kuongeza nguvu kwenye kipindi cha pili

Changamoto pekee inayoikabili Yanga huenda ikabaki kwenye safu ya ulinzi baada ya kukosekana kwa Andrew Vicent ambaye ni majeruhi na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliyefungiwa michezo mitatu

Kocha Noel Mwandila huenda akalazimika kumtumia kiraka Said Juma Makapu kwenye nafasi ya ulinzi sambamba na mkongwe Kelvin Yondani.

Pia yupo beki aliyepandishwa kutoka Yanga B Cleosaf Sospeter

Kamati ya saidia Stars ishinde yakutana Dar

Hivi karibuni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliunda Kamati maalum ya kusaidia Taifa Stars ishinde mchezo dhidi ya Uganda utakaopigwa March 24 ili iweze kutinga fainali za AFCON zitakazofanyika nchini Misri baadae mwaka huu

Kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh Paul Makonda leo ilikutana katika kikao chake cha pili kilichofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam

Kamati hiyo ina wajumbe 14.

Djuma aitakia kheri Simba

Kocha Mkuu wa AS Kigali inayoshiriki ligi kuu ya Rwanda, Masudi Djuma ameitakia kheri Simba ili iweze kushinda mchezo dhidi ya AS Vita Club na kuweza kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Djuma aliyewahi kuhudumu Simba akiwa kocha msaidizi kwa misimu miwili, amesema Simba itakayokuwa nyumbani ina kila sababu ya kushinda mchezo huo Jumamosi

“Timu zinazoshiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu zimetumia vyema viwanja vyao vya nyumbani. Naamini Simba itatumia uwanja wake vizuri pia,” Djuma aliiambia Radio eFM

Djuma aliondolewa Simba mwezi Oktoba mwaka jana baada ya kutofautiana na kocha Mkuu Patrick Aussems.

Nafasi yake tayari imechukuliwa na kocha Denis Kitambi

Djuma anabaki kuwa miongoni mwa makocha waliopita Simba na kukubalika sana na mashabiki wa timu hiyo

Aussems amewapania kwelikweli AS Vita

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wanayo kila sababu ya kushinda mchezo wa keshokutwa dhidi ya AS Vita utakaopigwa saa moja usiku katika uwanja wa Taifa

Aussems ambaye msimu huu ameiongoza Simba kwa mafanikio makubwa kwa kuweza kuipeleka hatua ya makundi, amedhamiria kuvuka malengo kwa kutinga robo fainali

“Mchezo huu muhimu kuchezwa katika uwanja wetu wa nyumbani mbele ya mashabiki wetu, inatuongezea kujiamini.

“Tuko katika nafasi nzuri zaidi ya kupata ushindi kuliko wapinzani wetu,” amesema Aussems

“Nafahamu mchezo hautakuwa mwepesi kwani wapinzani wetu nao wanahitaji ushindi ili wafuzu”

“Lakini sisi tuna faida ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa mashabiki wetu. Ni muhimu mashabiki wakajitokeza kwa wingi uwanjani, wajaze uwanja na watuunge mkono kwa muda wote wa mchezo, ushindi utakuwa upande wetu”

Mshindi wa mchezo kati ya Simba dhidi ya AS Vita atajihakikishia kutinga hatua ya robo fainali na timu itakayoshinda kwenye mchezo kati ya Al Ahly dhidi ya JS Saoura unaopigwa Misri

Matokeo ya sare yatazipa nafasi JS Saoura na Al Ahly kutinga robo fainali

Niko fiti kuwakabili AS Vita – Wawa

Beki kisiki wa Simba Paschal Serge Wawa amesema yuko imara kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS Vital utakaopigwa keshokutwa Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa

Wawa alipata majeraha ya kifundo cha mguu kwenye mchezo uliopita dhidi ya JS Saoura ambapo Daktari wa Simba Yassin Gembe alisema beki huyo raia wa Ivory Coast pamoja na kiungo Haruna Niyonzima walipata majeraha ya enka kutokana na mazingira ya uwanja wa Agosti 20 ambao una nyasi bandia

Wawa amesema hali yako imeimarika na atacheza mchezo wa Jumamosi

“Niko vizuri sasa, niliumia katika mechi iliyopita kule Algeria, lakini sasa ninaendelea vizuri na nitacheza mechi ya Jumamosi,” amesema

“Naamini tutafanya vizuri kwenye mchezo huo, tutapambana kwa sababu tunataka kuwafurahisha mashabiki wetu na vilevile tunataka kuweka rekodi ya kutinga robo fainali”

Wawa alishiriki mazoezi ya Simba yliyofanyika kwenye uwanja wa Boko Veterans jana jioni